The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: 27 AGOSTI, 2018. .


Ziara ya Mkurugenzi Mtendaji  nchini Korea Kusini na China

Kati ya tarehe 10-18, Agosti 2018 Mkurugenzi Mtendaji Bw. Geoffrey Mwambe alifanya ziara ya kikazi nchini Korea ya Kusini na China ili kuhamasisha na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta ya Afya hususani ujenzi wa viwanda vya kutengeneza madawa na vifaa tiba. Katika ziara hiyo Bw. Mwambe aliongoza  msafara kwa upande wa Korea Kusini uliojumuisha wawakilishi wa Taasisi za Serikali, Makampuni binafsi na Viongozi wa Chama cha Watengenezaji na Wauzaji wa Madawa ‘Association of Pharmaceutical Industries’ (TAPI) 15 ili kushiriki kongamano la biashara na uwekezaji  lililofanyika tarehe 13 Agosti  huko Korea ya Kusini. Aidha msafara wa nchini China uliongozwa na Mhe. Ummy Mwalimu (MB) Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambapo pia walishiriki kongamno la biashara na uwekezaji lililofanyika huko Beijing, China tarehe 16 Agosti,2018. Lengo kuu la kushiriki makongamano hayo ilikuwa ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa nchi  hizi,  kujadili fursa za uwekezaji/ubia katika sekta ya madawa na vifaa tiba.  Makongamano yaliambatana na ziara za kutembelea viwanda vinavyomilikiwa na baadhi ya makampuni yaliyoonesha nia ya kuja kuwekeza nchini. Shukrani za pekee ziwaendee waheshimiwa mabalozi wetu kwa kufanikisha makongamano hayo yenye lengo la kuleta mapinduzi ya uchumi Tanzania. Mabalozi hao ni Mhe. Matilda Masuka (Korea Kusini) na Mhe. Mbelwa Kairuki (China). Mafanikio yaliyopatikana kutokana na ziara hizo ni pamoja na makampuni matano kuonesha nia ya kuja kuwekeza nchini kwenye viwanda vya kutengeneza madawa na vifaa tiba, na kusainiwa kwa Hati za Maafikiano  (MOU)  tatu kati ya TAPI na wafanyabiashara wa makampuni ya China ili kuwezesha mashirikiano na makampuni ya Tanzania kuwekeza kwa ubia katika sekta ya afya.

 

   Ushindi wa TIC kwenye Maonesho ya Nanenane, 2018

Ndugu Wadau,Tunapenda kuwajulisha Wananchi kuwa Ofisi za Kanda za TIC saba zilishiriki maonesho ya Wakulima ‘Nanenane’ yaliyofanyika kanda mbalimbali nchini katika Mikoa ya Simiyu, Arusha, Lindi, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Tabora. Kati  ya Ofisi zetu hizo za Kanda, tatu zimeibuka na tuzo za ushindi. Ofisi zilizopata tuzo ni Kanda ya Kusini (Mtwara) iliyoibuka mshindi wa pili kwenye kundi la Taasisi za Huduma na Utafiti na kutuzwa Kombe, Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam) iliyopata pia ushindi wa Pili katika kundi la Taasisi za Kiuchumi  na kutuzwa Cheti na ushindi wa tatu ulipatikana kupitia Kanda ya Kati (Dodoma) iliyoibuka mshindi wa pili katika kundi la Taasisi za Kiuchumi na kutuzwa Cheti. Ushindi huo ni mafanikio kwa Taasisi ambapo imetambulisha Ofisi zake za Kanda na kutoa elimu kwa Umma kuwa huduma za TIC kwa sasa zinapatikana kupitia ofisi zetu za Kanda tofauti na awali ambapo huduma hizi zilikuwa zikipatikana Makao Makuu  yaliyopo Dar es Salaam tu. Tunatoa wito kwa Umma, Viongozi, Wananchi na jamii waweze kutumia Ofisi zetu za Kanda kupata huduma zinazotolewa na TIC.  Ofisi hizi  na mahali zilipo ni Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam,  Jengo la Mkuu wa Mkoa) , Kanda ya Kati (Dodoma, Jengo la CDA), Kanda ya Ziwa (Mwanza, Barabara ya Kenyatta), Kanda ya Kusini ( Mtwara, Jengo la Mkuu Mkoa), Kanda ya Kaskazini (Moshi, Jengo la KAIDC), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ( Mbeya, Jengo la NBC) na Kanda ya Magharibi ( Kigoma Jengo la Mkuu wa Mkoa).

 

   Ujio wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)

Ndugu Wadau, Kituo cha uwekezaji kinaendelea Kuboresha Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre) ili kuwahudumia wawekezaji kwa ufanisi zaidi. Katika jitihada hizo hivi karibuni,  Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imejumuika na taasisi nyingine za serikali ambazo tayari zipo TIC ili kuhdumia wawekezaji. Taasisi nyingine ndani ya TIC ni Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS), Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Ardhi, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu. Jukumu la kubwa la NIDA ni kusajili na kutoa vitambulisho kwa wawekezaji wazawa na wageni, wafanyakazi na wategemezi wao. Hivyo, tunawakaribisha wadau wetu kupata huduma za NIDA ndani ya ofisi za TIC.

 

Ndugu wadau, vilevile leo pia tunawataarifu kwamba TIC inazindua mfumo wa ndani wa Ki-Electronic wa kutoa vibali vya kazi kwa wawekezaji. Kwa utaratibu huu nyaraka za maombi yote ya vibali hivyo yatatakiwa kuwasilishwa katika mfumo wa ‘soft & hard copies’ kuanzia tarehe 3 Septemba, 2018.

  

  Mchango wa TIC katika kuwajenga Wajasiriamali (SMEs)

Ndugu Wadau, Uwekezaji ndiyo njia sahihi ya kufikia uchumi wa viwanda. Kwa kuzingatia hilo, ni wazi kwamba tuna jukumu la kuijenga sekta binafsi ambayo ni nyenzo kuu katika uwekezaji/ kujenga uchumi. Vilevile suala la kujenga sekta binafsi iliyo imara haliepukiki kwani limedhamiriwa na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli inayojipambanua kuwasaidia Watanzania na kuwataka washiriki katika kujenga uchumi wao. Katika, kutekeleza hilo, Kituo kimejipanga kuwapatia elimu Wajasiriamali (SMEs) ili waweze kushiriki kutengeneza mifumo itakayowasaidia kama Wazawa kuweza kukua na kuchukua nafasi ya uwekezaji ndani ya nchi yao. Vilevile, msukumo wa Kituo kwa sasa ni kuwaelimisha Wajasiriamali wafanye shughuli zao za kiuchumi kwa ubunifu ili waweze kumudu mahitaji ya wawekezaji wakubwa hususani kuwapatia huduma katika nyanja za biashara na uwekezaji. Mwisho, Kituo kinawapa hamasa Wajasiriamali (SME) waweze kuzalisha bidhaa zao wakilenga upatikanaji wa malighafi za kulisha viwanda tunapoelekea katika kujenga uchumi wa viwanda.

 

  Ushirikiano wa TIC, Taasisi mbalimbali za Serikali, Sekta Binafsi na Wananchi

Ndugu Wadau, Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba viongozi wa taasisi mbalimbali  za Serikali, Sekta Binafsi na Wananchi kwa ujumla kushirikisha Kituo cha Uwekezaji  Tanzania (TIC) pale wanaposhughulikia changamaoto mbalimbali zinazohusiana na uwekezaji ili Kituo kiweze kushauri njia bora za kushughulikia  changamoto hizo. Aidha tunawataka taasisi za serikalikutimiza wajibu waokwa wakati ili kuepushamalalamiko yasiyo na msingi na kuharibu taswira ya mazingira ya biashara na uwekezaji ya nchi yetu.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)