The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Uwekezaji wa kampuni ya HALO Group, kuleta mapinduzi chanya kwenye sekta ya ujenzi na uvuvi .


HALO Group ni kampuni ya Namibia ambayo ilianzishwa mwaka 2015 ikijihusisha na ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu. Viongozi wa kampuni hiyo wamefika nchini na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, Angellah Kairuki ambapo wameonesha nia ya kuwekeza kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba. Nyumba zitakazojengwa zitatumia teknolojia rahisi lakini bora, zenye gharama nafuu na zenye uwezo wa kudumu kwa muda mrefu. Mpango wa muda mrefu ni kujenga nyumba takribani milioni 3 katika Mikoa mbalimbali nchini..


Katika mzaungumzo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. Daniel Cullen pia ameeleza kuwa mpango wa pili wa kampuni ya HALO ni kuwekeza kwenye sekta ya uvuvi ambapo watawekeza kwenye kutengeneza boti za uvuvi. Boti hizo zitatengenezwa kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi katika sekta ya uvuvi nchini. Hta hivyo Bw. Cullen akifafanua amesema, ujio wa boti hizo utaenda sambamba na uanzishaji wa viwanda vya kuongeza thamani samaki, ufungashaji na uuzaji wa samaki ndani na nje ya nchi. Ili kufanikisha, kampuni imejipanga kufanya kazi kwa karibu na wadau wote wa uvuvi (wavuvi na viongozi). Aidha, kupitia mradi wa uvuvi, wavuvi pia watanufaika na mradi wa ujenzi wa nyumba lengo likiwa ni kuleta mabadiliko chanya sio tu katika sekta ya uvuvi lakini pia na kwa wavuvi wenyewe ikiwemo kuboresha hali zao za makazi, kuwa na soko la uhakika na kuinua pato lao.


Wawekezaji hao tayari wapo nchini wakiendelea kufanya mashauriano na Taasisi husika ili kuona namna ya kufanikisha uwekezaji huo kwa kuleta faida kwa pande zote (wawekezaji, Serikali na wavuvi kiujumla). Wawekezaji wameshauriwa kutekeleza mradi huo kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa vibali,vyeti na leseni zote muhimu.

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)