The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Tabia za kibinadamu walizonazo Faru Debora na Zawadi ni kivutio cha kipekee cha utalii na uwekezaji katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi .


Wilaya ya Same imetembelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC kujionea fursa za uwekezaji kwa ajili ya kuzinadi kwa wawekezaji. Same ina fursa nyingi ikiwemo Hifadhi ya Mkomazi ambayo awali ilikuwa pori la akiba kabla ya miaka ya 2008. Pori hili la akiba lilipendekezwa kuwa hifadhi ya Taifa kwa misingi ya kunusuru maeneo na rasilimali zilizomo kutokana na matumizi yasiyoendana na uhifadhi kwa ajili ya kizazi cha leo na kijacho. Katika hifadhi hii kuna wanyama na ndege wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na mbwa pori, vifaru weusi walioingizwa kutoka nchi ya Afrika Kusini, Uingereza na Jamhuri ya Czech. Pia hifadhi hii ina wanyama wakubwa watano wanaotambulika ulimwenguni kote (big five), ina maeneo ya milima na mabonde, ina maeneo ya kufanyia ‘picnic’, ina maeneo yenye mabwawa ambayo muda wote yanakuwa na wanyama wengi na wa aina mbalimbali, na ina miundo mbinu ambayo inamwezesha mtalii ama mwekezaji kufikia maeneo tofauti na kuendesha shughuli zake  bila kukwama.

 

Kipekee kabisa, mbuga ya Mkomazi inasimamia mradi wa kuzalisha /kuongeza idadi ya Faru weusi nchini ambao walikuwa hatarini kutoweka. Maradi huu wa aina yake ni kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi. Baadhi ya Faru wanaohifadhiwa Mkomazi, wamepewa majina ya binadamu na pia wamefundishwa tabia za kibinadamu ikiwemo kuitwa jina na kuitika, utii, kulishwa chakula kwa mkono na mambo mengine kama walivyoelekezwa na waangalizi wao jambo ambalo ni la nadra kutokea. Ukiwa mbuga ya Mkomazi, utakutana na Faru Debora na Faru Zawadi wakiwa na watoto wao. Hali hii inatajwa kuwa ni fursa nzuri na ya pekee kwa wageni wote kutoka mataifa mbalimbali kuja kujionea na kufanya utalii, alisema Kamishna Msaidizi wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Abel Mtui.

 

Akizungumza baada ya kutembelea mbuga hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe amejionea fursa nyingi ambazo kama nchi tunaweza kuzinadi ili kuvutia wawekezaji na watalii kutokana na uwepo wa hifadhi ya Mkomazi. Miongoni mwa fursa hizo ni utalii wa kuangalia ndege na wanyama  wa aina mbalimbali ikiwemo Faru ambao wamefundishwa tabia za kibinadamu, ujenzi wa hoteli, lodges,   kambi za kudumu za wageni‘permanent camps’(zitakazowezesha kutoa malazi kwa wageni watakotembelea maeneo ya hifadhi hiyo kuanzia 50) na pia kujionea safu za vilima na tambarare zinazotengeneza uoto wa asili wa nchi unaovutia kuangalia. Aidha Mwambe amesema ipo haja kwa Wadau wa utalii kuunganisha ‘holiday and tour package’ za hifadhi ya Taifa ya Mkomazi pamoja na ile ya utalii wa upandaji wa Mlima Kilimanjaro ili kuwezesha watalii wengi kuifahamu na kutembelea hifadhi ya Mkomazi. Hatua hii itasaidia kuleta watalii wengi ambao wataongeza tija ya kiuchumi (kwa Wana Hai, Mkoa na Taifa kwa ujumla) kutokana na mapato yatakayoingizwa.

 

Tayari maeneo yanayofaa kwa uwekezaji ndani ya mbuga yameainishwa na yapo tayari kwa mwekezaji yeyote mwenye nia ya kuendesha uwekezaji wake kwa kutumia miongozo na taratibu zilizowekwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA). Wadau wa utalii ndani na nje ya nchi wanakaribishwa kufanya utalii na uwekezaji katika hifadhi ya Mkomazi.

 

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)