The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Urahisishwaji wa utoaji huduma kwa wawekezaji ndani ya muda mfupi ni ufunguo wa milango ya kuvutia wawekezaji (wazawa na wageni) .


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Uwekezaji Bi. Doroth Mwaluko, amezisihi Taasisi za Serikali zinazofanya kazi kwenye mfumo wa Huduma za Mahala Pamoja, (One Stop Centre) ambao ni TRA, NEMC, UHAMIAJI, Wizara ya Kazi, NIDA,TBS,TMDA, ARDHI na  BRELA, kuzidi kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kurahisisha utoaji wa huduma zinazotakiwa na wawekezaji katika kufanikisha uwekezaji nchini. Katibu Mkuu amesema hayo alipotembelea na kuzungumza  na Menejimenti na Watumishi wa Kituo chini ya Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Maduhu Kazi. 

 

Urahisishwaji wa utoaji huduma kwa wawekezaji ndani ya muda mfupi unatafsiriwa kuwa ufunguo wa milango ya kuvutia wawekezaji (wazawa na wageni) zaidi na kufanya maamuzi na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali viwanda, utalii, madawa, kilimo, madini, uvuvi na ufugaji. Aidha, Katibu Mkuu amewataka Watumishi wote kufanya kazi kwa bidii, uwazi, ukweli na ufanisi kwa kulenga tija ya uwekezaji kwa nchi.

 

“Kama nchi, tunahitaji wawekezaji wazawa na wageni, lakini ujio wa wawekezaji hao unategemea namna tunavyofungua milango kwao kwa maana ya kurahisisha utoaji wa huduma zinazotakiwa katika kufanikisha uwekezaji wao hapa nchini. Kwa pamoja Taasisi/Mamlaka mshirikiane katika kuwafanikishia wawekezaji mahitaji yao kwa kufanya kazi kwa kasi, ukweli, uwazi na ufanisi zaidi’ amesema Katibu Mkuu Bi. Mwaluko katika ziara aliyoifanya Kituoni hapo. 

 

Aidha katika kuboresha mazingira ya uwekezaji Katibu Mkuu ameeleza kwamba, Serikali ya awamu ya tano ipo mstari wa mbele katika  kuboresha mazingira ya uwekezaji ambapo amesema wamedhamiria kuimarisha zaidi huduma za wawekezaji ikiwamo kuwezesha zaidi na kuboresha Mtendaji kazi katika Ofisi za Kanda za TIC, kufanikisha mfumo wa electronic single window kuanza, kuongeza uwajibikaji, kupunguza muda wa utoaji huduma (upatikanaji wa ardhi, vyeti, leseni na vibali) na kupiga vita rushwa. Yote hayo yatafanikiwa iwapo kila Taasisi itatambua kwamba  tunajenga nyumba moja na kwamba huduma yake ni nguzo muhimu katika kufanikisha uwekezaji kwa kushirikiana na Kituo.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt. Maduhu Kazi amempongeza Katibu Mkuu kwa ziara aliyoifanya Kituoni na kwamba maelekezo aliyoyatoa yamepokelewa na yatafanyiwa kazi. Aidha, Dkt. Maduhu ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu iendelee kushirikiana na Kituo katika jitihada za kuvutia uwekezaji na pia kuwahudumia kwa haraka ikiwemo kushughulikia changamoto zinazojitokeza.

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)