The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Wadau wa uwekezaji wamehimizwa kuwaona wawekezaji kama wabia, watu muhimu wanaokwenda kuzalisha ajira na kukuza pato la Taifa .


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji) Mhe. Prof. Kitila A.K.Mkumbo amefanya ziara katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Desemba, 2020.  Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kujifunza shughuli za TIC na kufanya vikao na Menejimenti na Watumishi ili kutoa mwelekeo wa Serikali kuhusu uwekezaji katika miaka mitano. Hii ni kufuatia kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji). Mhe Mkumbo amepokelewa na mwenyeji wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC,  Dkt. Maduhu Kazi.

 

Katika hotuba yake Mhe Mkumbo amemshukuru Mhe. Rais kumwamini na kumteua katika nafasi hiyo na kwamba atashirikiana na wadau katika kufanikisha uwekezaji nchini.

 

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Waziri amebainisha kuwa tayari Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia hotuba yake ya tarehe 13 Novemba, 2020 Jijini, Dodoma ameainisha malengo makuu uchumi. Akiyataja malengo hayo amesema ni kuwa na uchumi unaokua kwa asilimia 8 na pia kuzalisha ajira zisizopungua milioni 8 ndani ya miaka mitano. Vilevile Mhe. Waziri  amebainisha kwamba, Mhe.Rais pia alitoa njia ya kufikia malengo hayo kuwa ni kupitia wawekezaji wa ndani na nje. Hivyo uwekezaji ni nyenzo kuu katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

 

Kwa kuzingatia hayo, Mhe. Waziri ameelekeza Watumishi umuhimu wa kubadilisha mifumo ya utendaji na mitazamo ili kuwezesha nchi yetu inavutia uwekezaji mwingi kwa kadri iwezekanavyo kutoka nje na pia kuhamasisha wawekezaji wa ndani kuchukua nafasi za kuwekeza ili kukuza uchumi wa nchi. Pia Taasisi wadau wa uwekezaji wameelekezwa kuwahudumia wawekezaji kwa kuhakikisha kwamba mambo yote muhimu ya kuanzisha uwekezaji nchini yanakamilika ndani ya siku zisizopungua kumi na nne kama Mhe. Rais Dkt. Magufuli alivyoagiza katika Hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge.

 

Aidha, Mhe. Waziri amesisitiza Watumishi wa Umma kiujumla kuwaona wawekezaji kama  partners  huku akikemea tabia ya baadhi ya Watumishi kujiona maboss katika kuwahudumia wawekezaji. Watumishi wametakiwa kutoa huduma yenye ushawishi na mvuto kwa wawekezaji huku akiwataka kubadili mitazamo yao pale wanapokutana na wawekezaji walenge tu kuwapa taarifa na takwimu sahihi zitakazowasaidia kubaini iwapo vigezo vilivyowekwa wanakidhi ama hawakidhi.

 

‘Wawekezaji wanakuja na mitaji yao, wanachohitaji ni kupewa utaratibu unaoeleweka, usio na ubabaishaji ili wafanye maamuzi ya kuwekeza’, amesema Mhe. Mkumbo

 

TIC imehimizwa kujikita zaidi kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma walioko katika ngazi mbalimbali za Taifa, Mkoa, Wilaya na Halmashauri ili wajue kwamba kazi yao moja ya msingi ni kuwawezesha na kuwasidia watu na kampuni ambazo zinataka kuwekeza nchini, iwe kampuni ya ndani ama nje. Pia kwamba mwekezaji anapokuja na kuonana na Taasisi husika wasimuone kama mwana mpotevu badala yake mwekezaji aonwe kama ni mtu muhimu, ni mlipa kodi ajaye, mtu ambaye anakwenda kuzalisha ajira na anakwenda kukuza pato la Taifa.

 

Mhe. Mkumbo ametoa wito kwa wadau wa uwekezaji, Watumishi wa TIC na wale wanaohudumia wawekezaji kupitia Mfumo wa Mahala Pamoja, kutumia lugha nzuri kwa wawekezaji zenye lengo la kuvutia na kufanikisha uwekezaji  badala ya kutoa lugha kali zenye mlengo wa udhibiti. Mwisho amewakaribisha wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza kwenye sekta za kipaumbele ikiwemo kilimo, viwanda, uvuvi, ufugaji, nishati, utalii, miundombinu na kwamba Serikali ipo tayari kuwaunga mkono katika kufanikisha uwekezaji wao nchini.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)