The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Wafanyabiashara wadogo wadogo wa leo ndio wawekezaji wakubwa wa kesho. Wadau / Taasisi husika ni jukumu letu kuwasaidia kurasimisha biashara zao ili waende zaidi kwenye biashara ya viwanda vidogo vidogo vya utengenezaji na uzalishaji. .


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo amefanya ziara ya kutembelea Taasisi ambazo zinachagiza masuala ya uwekezaji nchini. Miongoni mwa Taasisi hizo ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Akizungumza katika Taasisi hiyo, Waziri ameupongeza uongozi wa Benki hiyo namna ambavyo umefanikisha upatikanaji wa mitaji kwa  miradi ya uwekezaji. Pamoja na pongezi hizo, Waziri ameitaka Benki hiyo kuongeza wigo wa kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, ili kuchochea ukuaji wa miradi ambayo baadae itapanuka na kua miradi mikubwa na yenye mchango mkubwa katika uchumi ikiwamo kutengeneza ajira.

 

Akizungumza katika kikao, Mhe. Waziri amesema, kuna haja ya kukuza wafanyabiashara wadogo wadogo kwa maslahi mapana ya ustawi wa Taifa letu. ‘Suala la kusukuma na kukuza wafanyabiashara wetu wadogo ni jukumu letu sote wadau na Taasisi zote wezeshi ikiwemo mabenki. Kwa taarifa zilizopo, zinaeleza kwamba Tanzania kuna wafanyabiashara wadogo takribani milioni 3.7, kati ya hao asilimia 73% wanajishughulisha na uuzaji na uchuuzi. Tafsiri yake ni kwamba wafanyabiashara hao hawazalishi isipokuwa wanauza mazao yanayozalishwa na watu wengine na katika bidhaa zinazouzwa na wafanyabiashara hao, zaidi ya asilimia 70 wanauza mazao yanayohusiana na kilimo’.

 

Kupitia maandiko mbalimbali, yanaonyesha kwamba mataifa makubwa ambayo leo yameendelea ikiwemo China na Korea yamefanikiwa baada ya kuweka nguvu kubwa katika kusaidia, kuinua na kuendeleza wafanyabiashara wadogo. Hakika sekta ya wafanyabiashara wadogo ikiboreshwa ni chachu ya ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote kwa kuwa kila nchi inatengeneza mabilionea wake kuanzia katika hatua ya wafanyabiashara wadogo na kati.

 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Waziri amehimiza wadau na Taasisi husika kuona kwamba kuna fursa kubwa moja kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ili biashara zao ziwe rasmi na pili kuwasukuma kimtaji, kitekinolojia na ushauri ili waende zaidi kwenye biashara ya viwanda vidogo vidogo vya utengenezaji na uzalishaji. Takwimu zinaeleza kwamba kwa sasa ni asilimia 3 tu ya wafanyabiashara wadogo wadogo wanaojihusisha na utengenezaji na uzalishaji. Nchi inataka wafanyabiashara wengi zaidi waingie kwenye fursa ya utengenezaji na uzalishaji katika sekta ya vipaumbele vya nchi ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji na uongezaji thamani. Kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzalisha ajira, amesema Waziri Mkumbo.

 

Wafanyabiashara wetu wadogo wengi wao wamejiajiri wenyewe, takwimu zinasema kuwa kati ya wafanyabiashara wadogo 10, kati yao 7 wamejiajiri wenyewe, lakini tukiwasukuma na kuingia eneo la uzalishaji na utengenezaji tunaweza kuwawezesha kuajiri angalau mtu moja ama wawili. Iwapo idadi ya wafanyabiashara wadogo tuliyo nayo yote itawezeshwa, ndani ya muda mfupi tutakuwa na nafasi ya kutengeneza ajira kwa watu wengi zaidi na hivyo kufanikisha Agenda ya Mhe. Rais ya kuzalisha ajira milioni 8 kutoka sekta isiyo rasmi, ameongeza Mhe. Waziri.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw. Japhet Justine amefurahishwa na ujio wa Mhe. Mkumbo na kueleza kwamba kazi ya Benki ya Kilimo ni kuandaa mitaji kwa ajili ya Watanzia ili wawekeze zaidi. Kwa kuzingatia hilo amemhakikishia Waziri na Serikali kiujumla kwamba wataendelea na kazi ya kutoa mitaji na kusapoti Watanzania kwa maendeleo ya Taifa katika sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo, ’conservation’ na uongezaji thamani.

 

Tangu benki hiyo ianzishwe, imetoa mikopo yenye thamani ya Tsh. bilioni 244 kwenye miradi ya uwekezaji ipatayo 210. Katika mwaka 2020 pekee, benki  imetoa takribani mikopo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 84. Sekta ya kilimo inakopesheka na marejesho yake ni mazuri tofauti na ilivyokuwa ikifikiriwa awali na wengi. Wakulima wanakopesheka kinachohitajika ni  kutoa muda wa kutosha kwa mkopo uliotolewa sambamba na msaada wa kitaalam kutegemeana na aina ya mradi ili kuwezesha mradi kuzalisha na kufanya marejesho husika. Benki ya TADB inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100% amesema Bwana Justine.

 

Taarifa ni fursa, washirika wa uwekezaji chukueni hatua ya kuwasiliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kupata taarifa zaidi ya aina ya miradi inayopata mikopo na vigezo vyake, kwa lengo la kupata mitaji ya kuendeleza miradi ya uwekezaji katika sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo, ’conservation’ na uongezaji thamani. Hatua hii itawezesha miradi ya uwekezaji kuongezeka sambamba na  uzalishaji, ajira, walipa kodi na pato la Taifa.

 

 

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)