The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Misri yafikiria kuwekeza kwenye mradi wa magari nchini hatua itakayosaidia kupunguza uingizaji wa magari (used cars) kutoka nje ya nchi. .


Ugeni wa takribani wafanyabiashara sita (6) kutoka Misri umefika nchini kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuanzisha uwekezaji wao hapa nchini. Ugeni huo ni kutoka kampuni ya Ghabbour Auto na umeongozwa na Dkt. Raof Ghabbour ambaye ni  Mkurugenzi  Mkuu na Mwenyekiti wa kampuni hiyo. Ukiwa nchini kwa niaba ya Waziri Mkuu, ugeni huo umepokelewa na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki Waziri Mkuu, Dar es Salaam leo tarehe 18 Septemba,2019. Kikao pia kimehudhuriwa na Maafisa kutoka TIC na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Kampuni ya Ghabbour Auto huko Misri inajishugulisha na uzalishaji wa magari, uunganishaji wa magari sambamba na uzalishaji wa spea za magari. Katika mazungumzo na Mhe. Kairuki,  Mwenyekiti Dkt. Raof amesema kampuni hiyo ina nia ya kuwekeza Tanzania kwenye eneo la kutengeneza magari na wataanza na mradi wa utengenezaji wa magari ya biashara (scania, trucks na tipper) au uunganishaji wa magari  na baadae kufuatiwa na mradi wa utengenezaji wa  magari ya abiria (passenger cars). Kwa kuzingatia hilo, Kampuni ya Ghabbour Auto imefika nchini ili kupata taarifa zaidi za kitaalamu na kufanya majadiliano na viongozi wa ngazi za juu ili kufahamu iwapo miradi ya aina hiyo ni kipaumbele kwa nchi, taratibu za kuanzisha miradi ya aina hiyo, aina ya msaada watakaopata kutoka Serikalini katika kufanikisha mradi huo, upatikanaji wa ardhi na aina ya misamaha ya  kodi itakayotolewa wakati wa kutekeleza mradi huo.

 

Akizungumza kwa niaba ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) Bw. John Mnali Mkurugenzi wa UHamasishaji Uwekzaji amewataarifu wawekezaji hao kuwa ,TIC kupitia Mfumo wa Mahala Pamoja umeanzishwa maalumu kwa ajili ya kuwasidia wawekezaji. Hivyo itasimamia na kufanikisha uanzishaji wa mradi huo kwa kutoa usaidizi wa aina yoyote utakaohitajika. Hii ni kuanzia hatua za awali za upatikanaji wa ardhi, usajili wa kampuni, cheti cha uwekezaji, masuala ya kikodi, vibali vya kazi na makazi pamoja na upatikanaji wa vyeti na leseni mbalimbali.

 

Naye Mhe. Kairuki akitoa majumuisho, amewakaribisha wawekezaji hao na kuwahakikishia kwamba maamuzi yao ya kuwekeza Tanzania ni sahihi. Hiyo ni kutokana na mazingira mazuri  ya biashara na uwekezaji yaliyopo na kuwa mazingira hayo yanaendelea kuboreshwa chini ya Rais wetu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Sambamba na uwepo wa mazingira mazuri, pia Mhe. Kairuki amewaelezea wawekezaji hao pia uwepo wa soko ambalo si tu la Tanzania bali pia la Afrika Mashariki. Aidha kipekee kabisa amewahakikishia wawekezaji hao utayari wa Serikali katika kufanikisha uwekezaji huo kwa kuwa ni muhimu kwa Taifa ikiwamo kutengeneza ajira, kuongeza pato la Taifa na kupunguza uingizaji wa magari (used cars) kutoka nje ya nchi.

 

Bw. Raof amefurahishwa na mazungumzo aliyofanya na Mhe. Waziri pamoja na timu yake ambapo ameahidi kutuma timu yake ya wataalamu kuja  nchini ili kuanza taratibu za kufanikisha uanzishaji wa maradi huo.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)