The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Wabunge wa Kamati mbili za Bunge walioshiriki semina ya TIC kuhusu masuala mbalimbali ya uwekezaji kuwa Mabalozi wa uwekezaji .


Wabunge wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma pamoja na Kamati ya Katiba na Sheria wamejengewa uwezo wa uelewa mpana wa masuala ya uwekezaji zoezi lililoendeshwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) huko Dodoma. Mgeni rasmi katika semina hiyo alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki. Semina ya TIC kwa Waheshimiwa Wabunge imeendeshwa ili kuwajengea uelewa mpana wa masuala ya uwekezaji hususan majukumu mbalimbali ya TIC kisheria. Majukumu hayo ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji (wazawa na wageni), huduma zinazotolewa kwa wawekezaji kupitia mfumo wa huduma za mahala pamoja (upatikanaji wa ardhi, idhini ya vibali, leseni na vyeti vya uwekezaji), kuishauri Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya uwekezaji nchini.

 

Akitoa neno katika semina hiyo, Mhe. Kairuki aliwaeleza Wabunge juu ya mikakati mbalimbali inayochukuliwa na Serkali kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na kupendekeza Sheria Mpya ya Uwekezaji sambamba na Sera ya Uwekezaji kwa kuwa zilizopo zina muda mrefu. Aidha, Waziri ametumia fursa hiyo kuwataarifu Wabunge ili wabaini jitihada za  kuboresha mazingira ya uwekezaji zinavyoendelea na kwamba wajiandae kuunga mkono Mswada wa Sheria Mpya utakapowasilishwa Bungeni. Semina pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TIC Prof. Longinus Rutasitara ambaye alieleza kuwa tofauti na zamani, kwa sasa uhamasishaji uwekezaji umelenga kuvutia zaidi wawekezaji wazawa.

 

Miongoni mwa mambo ambayo Wabunge wamenufaika kujifunza ni pamoja na namna Kituo kinavyoweza kuvutia uwekezaji kwa kuzingatia mahitaji ya mwekezaji (masoko, rasilimali, ardhi,), vigezo vya mwekezaji kujisajili na TIC, vivutio vya uwekezaji na nanmna vinavyovutia uwekezaji mpya, faida za uwekezaji, mwenendo wa nchi kidunia katika masuala ya uwekezaji, umuhimu wa huduma za mahala pamoja kwa mwekezaji na changamoto za uwekezaji kiujumla. Elimu kwa Wabunge iliwasilishwa na Mkurgenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Geoffrey Mwambe kwa njia ya mada.

 

Kwa upande wa Wabunge washiriki, wamepata fursa ya kujifunza zaidi juu ya masuala ya uwekezaji, kuwasilisha hoja za masuala ya uwekezaji zilizotolewa ufafanuzi kutoka TIC, kutoa maoni ya kuboresha mazingira ya uwekezaji, kutoa mtazamo wao juu ya kuiimarisha TIC ili iweze kuwa na nguvu zaidi ya kusimamia masuala ya uwekezaji nchini na kuwasilisha ushauri juu ya kutatua changamoto za uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi.

 

Katika majumuisho, Dkt. Raphael Chegeni ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma amesema kwa pamoja wameelewa mahitaji, mwenendo na nafasi ya Tanzania kiuwekezaji duniani. Aidha, amebainisha kuwa ingawa tayari kuna mikakati na jitihada zinazochukuliwa na serikali za kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi, kama nchi kuna haja ya kuharakisha utekelezaji huo. Dkt. Chegeni ameongezea kuwa baada ya uelewa walioupata kupitia semina, watakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuchangia hoja za uwekezaji zitakapowasilishwa bungeni. Naye Mhe. Dkt. Susan Kolimba ametoa pongezi kwa TIC kufanikisha semina hiyo na kwamba wamejengewa uwezo wa kuwa mabalozi wazuri wa uwekezaji. Hivyo, wataungana na TIC katika harakati za kuhamasisha na kuvutia uwekezaji zaidi nchini.

 

Zoezi la Kituo cha Uwekezaji Tanzania kutoa elimu ya uwekezaji ni endelevu na limelenga kuwafikia wadau wa kada mbalimbali nchini.

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)