The United Republic of Tanzania

TANZANIA INVESTMENT CENTRE

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesaini makubaliano na Baraza la Biashara la Uholanzi-Afrika (NABC) .


Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetiliana saini makubaliano ya mashirikiano na Baraza la Biashara la Uholanzi-Afrika (NABC) Novemba 20, 2019 katika Ofisi za TIC, Dar es Salaam.Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geoffrey Mwambe na Mkurugenzi Mkuu wa NABC Bw. Peter Ruiter na yamelenga kujenga mfumo wa pamoja wa kufanikisha biashara na uwekezaji zaidi baina ya Tanzania na Uholanzi. Maafikiano ya makubaliano hayo ni matokeo ya mkutano uliofanyika kati ya TIC na NABC nchini Uholanzi, Februari, 2019. NABC ina makampuni wanachama zaidi ya 300 ambayo yamewekeza katika sekta mbalimbali nchini Uholanzi. Sekta hizo ni pamoja na kilimo na kuongeza thamani, viwanda (nguo, maziwa), afya nishati, bandari, ujenzi, mifugo na kuongeza thamani.

 

Akizungumza mara baada ya kutiliana saini Bw. Mwambe amesema, makubaliano hayo yana tija kwa kuwa sasa Tanzania itaweza kutangazwa nje ya nchi kupitia mitandao ya NABC na mitandao mingine nchini Uholanzi. Hatua hiyo itasaidia kuongeza imani kwa wafanyabiashara na wawekezaji wananchama wa NABC na Ulaya kuwa Tanzania ni nchi nzuri ya kuwekeza pamoja na kushawishika kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali. Aidha, Mwambe ameongeza kuwa makubaliano hayo pia yatawezesha kufanyika kwa makongamano ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi kwa lengo la kufanikisha uwekezaji wa ubia, ajira, upatikanaji wa mitaji, teknolojia, utaalam na masoko. Pia Bw. Geoffrey Mwambe ameongezea kuwa Serikali inasimamia sera na Sheria za Uwekezaji ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hatua ambayo inazidi kuimarisha na kuiweka nchini kuwa sehemu nzuri ya uwekezaji. “Haya mnayoyaona yanatokana na usimamizi madhubuti wa Sera na Sheria za uwekezaji ambazo Tanzania imejiwekea, tunafanya hivi ili kuwa na uwekezaji wenye tija” alisema Bw. Mwambe.

 

Naye Bw. Ruiter amesema kupitia makubaliano waliyoingia na TIC, Tanzania itakuwa na nafasi nzuri ya kujitangaza Uholanzi na Ulaya kwa ujumla kwa sababu NABC itahamasisha na kushawishi wanachama wake kuchangamkia fursa zilizoko Tanzania kwa maendeleo ya nchi zote. Bw. Ruter amesema Uholanzi ni nchi ya kibiashara na uwekezaji hatua ambayo imewezesha kujenga uchumi wake. Hivyo, anatarajia makubaliano hayo yatatekelezwa kwa malengo ya kufanikisha biashara na uwekezaji ili kuinua zaidi uchumi wa Tanzania na watu wake. Bw. Peter akielezea ni kwa nini wameichagua nchi ya Tanzania amesema kuwa ni kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hususan amani. “Huwezi kufanya uwekezaji kwenye nchi ambayo haijatulia, mazingira yake hayapo sawa na uchumi wake haulindwi, Tanzania ni nchi nzuri sana na tunaweza kuwekeza hapa”alisema Bw. Peter de Ruiter.

 

Vilevile,Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo pia amesema uwekezaji Tanzania una manufaa makubwa kutokana na kuwa na uchumi usioyumba, mapambano dhidi ya rushwa na usimamizi mzuri wa rasilimali za nchi. Ruiter pia amesifu hali nzuri ya hewa ya Tanzania kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara na kuongeza kuwa ni muhimu kwa raia wa Uholanzi kuwekeza kwenye sekta hiyo. Baraza la Biashara la Uholanzi-Afrika NABC limesema linaangalia uwezekano wa kushawishi wawekezaji wa Uholanzi kuwekeza Tanzania kutokana na kuwepo kwa fursa mbalimbali zikiwepo Ardhi kwa ajili ya viwanda na kilimo

 

Bw.Mwambe amepongeza Ofisi za Ubalozi wetu nchini Uholazi chini ya Balozi Mhe. Irene Kasyanju kwa kufanikisha kutiliana saini makubaliano hayo yenye mlengo wa kuleta matokeo chanya kwenye nyanja ya uwekezaji/biashara nchini.

 

Social Medias

Copyright ©2018 Tanzania Investment Centre.
All Rights Reserved.
Designed, Developed, and Maintained by Tanzania Investment Centre(TIC)